Simba yaingia mkataba ‘mnono’ na EAG Group Limited
Klabu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’ Simba, leo imeingia mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya EAG Group Limited ambao utahusika na masuala ya kuitafutia dili za kuiingiza pesa klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurungezi wa EAG Imani Kajula amesema kuwa, mipango yote ya kuendesha dili hilo anaipata kutoka katika Klabu ya Arsenal ya England ambayo anafanya nayo kazi.
Kajula amesema katika mkataba huo anataka kuiona Simba inakuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa kuitafutia vyanzo vingi vya mapato ili iache kutegemea mapato ya mlangoni na ada ya wanachama pekee.
Naye rais wa klabu hiyo Evans Aveva amesema, anaamini mpango huo utawawezesha kuendeleza jengo lao la makao makuu liliopo Mtaa wa Msimbazi jijini Dar.
Aidha katika hatua nyingine, klabu hiyo imetangaza kuwa kila mwisho wa msimu itakuwa inamtangaza mchezaji wao bora wa klabu kwa mwaka ambapo atazawadiwa zawadi ya gari la kisasa huku mchezaji bora kijana akipewa pesa shilingi milioni tano na mchezaji mwenye nidhamu atapokea milioni mbili.
Amesisitiza kuwa washindi hao wote kila mmoja pia atazawadiwa simu ya kisasa aina ya Huawei Ascend Mate 7 yenye thamani ya shilingi milioni moja na nusu kutoka kampuni ya Huawei ambayo wameingia udhamini na klabu hiyo.