Tishio la Ugaidi: Jeshi la Polisi laimarisha Ulinzi Dar es salaam
Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es salaam limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jijini la Dar es salaam kufuatia kuwepo kwa taishio la kutokea ugaidi katika mikoa ya Dar es salaam na Mwanza.
Akizungumza na Mtandao wa Hivisasa Kamanda wa Kanda maalumu ya Dar es salaam Suleiman Kova amesema kwamba hali ya usalama ni shwari na kuahidi kuongeza opereshini ya kukamata wauza dawa za kulevya, wahalifu na pamoja na kulinda maeneo ya fukwe ambayo ni vichochoro vya matukio ya kihalifu.
Ameongeza kuwa Jeshi hilo limejipanga kukabiliana na vitendo vya kigaidi ambapo wanafanya uchunguzi kila mahali kwa kutumia vikosi vya mbwa, farasi, helkopta, magari, pikipiki na kutembea kwa miguu katika maeneo yote ya jiji.
Tishio la kigaidi nchini Tanzania linafuatia tukio la kukamatwa mtanzania nchini Kenya anayedaiwa kuwa ni mmoja wa magaidi walio wauwa takribani wanafunzi 148 katika chuo kikuu cha Garissa.