Zitto ajibu mapigo, awataja maadui wa ACT
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amewataja maadui zake pamoja na watu wasiokitakia mema chama cha kipya katika medani za siasa ACT-Wazalendo.
Akiuhutuba mamia ya wananchi jana katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza Zitto amesema kadri siku zinavyosonga wabaya wake wamekuwa wakijionyesha. Pamoja na hali hiyo ACT-Wazalendo haiko tayari kuzungumzia siasa za wakati uliopita kwa vile kufanya hivyo si afya njema kwa siasa za upinzani.
Amesema ni vema viongozi wa vyama vya upinzani waachane na ugomvi binafsi na watangulize masilahi ya taifa mbele, wao (ACT) wana nia ya dhati lakini wenzao wanaweka ugomvi binafsi mbele ya masilahi ya taifa.
“Mwanzo walipotufukuza walituambia tukatafute vyama vingine hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa wakasema vipo kwa ajili ya kugawa upinzani tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuiondoa CCM…wenzetu pia hili hawalitaki,” amesema Zitto.
Amesisitiza kuwa hakufundishwa kugombana na watu barabarani au kusema ovyo mitaani, kufanya hivi hakuna tofauti na kumsema mke au mume mlioachana.
Akizungumzia ujamaa amesema ujamaa haina maana kuwa chama hicho kitataifisha mali za watu, bali kitarekebisha makosa ya ubinafsishaji kwa kurejesha mali zote za taifa zilizouzwa na wanunuzi hawajatekeleza mikataba yao.
Chama cha ACT-wazalendo leo kinatarajia kuendelea na ziara yake Musoma baada ya kufanya mikutano katika mikoa ya Ruvuma,Singida na Tabora.