Friday, 26 May 2017

Sakata La Mchanga Wa Madini, Kigogo TMAA Ajisalimisha Takukuru

Mtendaji Mkuu wa TMAA  Dominic Rwekaza.

IMG-20170426-WA0006

Mtendaji Mkuu wa TMAA Dominic Rwekaza. Mtendaji Mkuu wa TMAA aliyesimamishwa kazi na Rais Dkt.John Pombe Magufuli Dominic Rwekaza anadaiwa kuripoti katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini Dar es salaam jana.

Kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka ndani ya Takukuru kimebainisha kuwa Kigogo huyo amefika katika taasisi hiyo kwa mahojiano kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo sekta ya Madini hivyo kupelekea nchi kupata hasara.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola amesema watendaji wote wanaodaiwa kuhusika katika sakata la kuzembea kudhibiti biashara ya kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi, watachunguzwa na taasisi yake.

Mlowola aliongeza kuwa watendaji ambao walihusika kwenye sakata hilo na sasa hivi hawapo madarakani au wanashikilia nyadhifa nyingine, nao lazima watahojiwa na taasisi hiyo ili kufahamu sababu ya kuruhusu taifa kupata hasara kubwa kiasi hicho.

Watendaji hao ni wanaofanya kazi Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), Wizara ya Nishati na Madini na taasisi nyingine zinazohusika na madini.

“Maelekezo ya Rais yalikuwa wazi kabisa kwetu na sisi tumeshaanza uchunguzi wetu,” alifafanua Mlowola.

Rais Magufuli aliagiza vyombo vya dola kuwachunguza Mtendaji Mkuu wa TMAA, Rwekaza na watendaji wengine wanaohusika na eneo hilo la usafirishaji makinikia.

Sakata la mchanga wa dhahabu pia limeng’oa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwa kushindwa kujenga kinu cha kuchenjulia mchanga wenye mchanganyiko wa madini.

clouds stream