Tuesday, 26 September 2017

Abiria Wanusurika Kufa Baada Ya Basi Kuteketea Moto Barabarani



Abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Tanga kuelekea Jijini Dar es salaam wamenusurika kufa baada ya basi walilokuwa wamepanda
la Kampuni ya Tashriff kuteketea kwa moto.
Mashuhuda wa tukio hilo wamedai kuwa waliona moshi ukitoka chini ya basi hilo ndipo wakapiga kelele na kusababisha dereva
kusimama dakika chache baada ya hapo likaanza kuwaka moto.
“Tulisikia kelele kutoka kwa watu waliokuwa nje tukaona dereva kasimamisha basi muda si mrefu moshi ulianza kutoka mara
moto ukalipuka,” abiria mmoja aliyesafiri na basi hilo amenukuliwa akisema.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amethibitisha kutokea kwa ajali majira ya saa nane mchana katikaeneo la Pongwe nje kidogo ya Jiji la Tanga.
Kamanda Wakulyamba amesema basi hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa na Hemed Ali (35) lilikuwa na abiria 29 ambapo hakuna
aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha.
“Hakuna aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha, abiria wote walitoka salama isipokuwa mizigo na mali zao zote zimeteketea moto,”ameongeza.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha moto huo katika ajali hiyo.

clouds stream