Friday 29 September 2017

WAZIRI,WABUNGE 25 AKIWEMO BOBI WINE WAPIGWA ‘STOP’ UGANDA





Spika wa Bunge la Uganda Rebecca Kadaga amewasimamisha Waziri mmoja na wabunge 25 kuhudhuria vikao vya bunge kwa
madai ya kushiriki katika vurugu ambayo ilimlazimisha kuahirisha kikao siku ya Jumatano.
Mmoja wa waliozuiliwa kuhudhuria vikao ni Waziri wa Maji, Ronald Kibuule kwa madai ya kwenda katika ukumbi wa bunge akiwa
na silaha.
Wabunge wengine waliosimamishwa kuhudhuria vikao wengi wao ni wa upinzani wanaopinga kufutwa kwa kifungu 102(b) kutoka
katika katiba ambayo inakataza watu ambao wana umri zaidi ya miaka 75 kugombea nafasi ya urais, ambao siku ya jana
walikataa kutoka katika ukumbi wa bunge na kumlazimisha spika kuahirisha kikao.
Miongoni mwa waliozuiwa kuhudhuria vikao vya bunge ni pamoja Robert Kyagulanyi a.k.a Bobi Wine (Kyaddondo Mashariki), MP
Allan Ssewanyana (Makindye Magharibi), Monica Amoding (Wilaya ya Kumi ), Dkt. Sam Lyomoki (Wafanyakazi) Betty Nambooze
(Manispaa ya Mukono) Ibrahim Kasozi (Makindye Mashariki) na Moses Kasibante (Rubaga Magharibi).
Baada ya mgogoro huo, maafisa wa ulinzi wakiwa katika vazi la suti walivamia Ukumbi huo na kuwalazimisha Kyagulanya na
Ssewanyana kutoka nje.
Serikali ya Uganda inataka kuondoa ukomo wa umri kwa wagombea urais kitu kilicholeta vurugu Jumatano katika Bunge la
Uganda baada ya Spika kuanza kuzungumzia suala hilo.
Hatua hiyo ya Serikali itamwezesha Rais, Yoweri Museveni kuendelea na nafasi yake ya urais na kugombea katika uchaguzi ujao.
Sheria hizo zilikuwa tayari zimebadilishwa mwaka 2005 zikiondoa ukomo wa awamu mbili ambapo ilimwezesha Museveni ambaye
sasa ana umri wa miaka 72 kuendelea kuwepo madarakani akiwa anahudumu awamu yake ya tano sasa.
Chini ya katiba iliyokuwepo Rais Museveni atakuwa amepitiliza umri unaoruhusiwa na katiba kugombea katika uchaguzi wa
mwaka 2021.

clouds stream