Tuesday, 26 September 2017

Jeshi La Polisi Lasema Haya Kuhusu Maiti 3 Zilizokutwa Coco Beach


Jeshi la Polisi limesema kuwa bado halijapelekewa uthibitisho kuhusiana na maiti za wanaume watatu waliokutwa pembezoni
mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach ili liweze kutolea ufafanuzi.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema iwapo atapelekewa udhibitisho huo ni lazima
atatolea ufafanuzi suala hilo kiundani zaidi.
“Sijaletewa ‘fact’ nikiletewa nitalitolea ufafanuzi,” amesema Kamanda Mambosasa.
Maiti za watu hao zilikutwa juzi Septemba 24 huku mbili zikiwa zimefungwa kwenye viroba na nyingine ikiwa imekutwa na jiwe
kubwa lililofungwa na kamba.
Maiti hizo ziligunduliwa na wafanyabiashara wa mihogo wa eneo hilo waliokuwa katika biashara zao asubuhi na ghafla waliona
maiti moja ikielea karibu na miti aina ya mikoko ikiwa na jiwe lililofungwa kifuani huku mikono yake ikiwa imefungwa na kamba.
Mmoja wa wafanyabiashara, Aziza Ally amesema baada ya kuona maiti hiyo walitoa taarifa polisi ambapo walifika saa 4 asubuhi
na kuichukua kwenye gari lao.
Amesema ilipofika saa 8 mchana waliona maiti mbili kila moja ikiwa kwenye kiroba zikielea ndipo mmoja wao alipoamua kutoa
taarifa polisi baadaye zikachukuliwa.
“Polisi walipokuja kuchukua hizi maiti hakuna hata mtu mmoja aliyeruhusiwa kusogelea na kupiga picha tulishangaa sana kuona
ulinzi mkali tofauti na siku zote na aliyebainika amepiga alipokonywa simu yake,” amesema Ally.

clouds stream