Tuesday, 27 October 2015

Ezekiel Wenje aangukia pua Nyamagana, adai demokrasia haijatendeka

Ezekiel Wenje aangukia pua Nyamagana, adai demokrasia haijatendeka

Tarehe October 27, 2015
Ezekiel Wenje akiongea na waandishi wa habari.
Mgombea wa Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Jimbo la
Nyamagana Mkoani Mwanza, ameibuka mshindi wa kiti cha Ubunge katika jimbo hilo na kumbwaga aliekuwa mbunge wa jimbo hilo Ezekiel Wenje, kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘Chadema’.
Katika matokeo hayo Stanslaus Mabula ameibuka kidedea kwa kupata kura 81,017 na hivyo Ezekiel Wenje, kupata kura 79,280.
Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi mkuu wa uchaguzi jimboni Tito Mahinya, huku kukiwa na ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama katika viunga vya ofisi za Jiji hilo.
Akitakangaza matokeo hayo majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo, Mahinya, alibainisha kuwa pia CCM imeibuka kidedea kwa upande wa Madiwani ambapo kati ya Kata 18, imeshinda Kata 14 na Chadema Kata nne.
Kwa upande wa Wagombea wengine, Chacha Okong’o (ACT Wazalendo) alipata kura 161, Faida Potea (CUF) amepata kura 1,005, Ahmad Mkangwa (NRA) kura 104, Mohamed Msanya (Jahazi Asilia) kura 175 na Ramadhan Mtoro (UDP) amepata kura 68. Hata hivyo kabla ya matokeo hayo kutangzwa, mgombea kutoka Chadema, Ezekiel Wenje, alikataa kusaini karatasi ya wagombea na kubainisha
kuwa demokrasia haikutumika katika zoezi zima la kuhesabu kura katika
uchaguzi huo na kwamba atafuata hatua zaidi za kisheria katika kupinga matokeo hayo.
Kwa upande wake Mshindi wa Uchaguzi huo Stanslaus Mabula, amesema kuwa tangu awali alitarajia ushindi huo na kwamba suala la demokrasia limezingatiwa.
Katika hatua nyingine Mabula, amedai kuwa atahakikisha anatatua changamoto zinazolikabili Jiji la Mwanza, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wakazi wa Jiji katika shughuli mbalimbali za uzalishaji ili waweze kujitegemea kiuchumi.

clouds stream