Friday 16 October 2015

Tazara ‘Flyover’ kugharimu Bilioni 100


Tazara ‘Flyover’ kugharimu Bilioni 100




Barabara ya Juu ‘Flyover’ inavyotarajiwa kuwa ikikamilika.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Japan, zimewekeana saini mkataba wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 100, kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa barabara ya juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mgombea wa Nafasi ya Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameeleza kuwa fedha hizo zinatokana na msaada wa shilingi bilioni 93.438 kutoka Serikali ya Japan huku Serikali ya Tanzania ikichangia shilingi bilioni 8.26.
Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa hatua hio ya utiaji saini ni faraja kubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam, kwa kuwa mradi huo wa ujenzi wa ‘flyover’ utasaidia katika kupunguza kero ya msongamano wa magari jijini.
Aidha amesema kuwa Serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Serikali ya Tanzania, katika kuleta maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali ya barabara na madaraja ikiwemo barabara ya Mwenge kwenda Tegeta, mradi uliogharimu shilingi bilioni 88, Mwenge kwenda Morocco ambayo ipo katika mkakati, pamoja na mradi wa ‘flyover’ wa Mbagala Rangi tatu kwenda Tazara.
Pia Mhe. Dkt. Magufuli ameeleza kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha inawaunganisha wananchi wake kupitia mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami, ili kurahisisha mawasiliano na usafirishaji wa watu, bidhaa na biashara kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale, ameeleza kufurahishwa na hatua hiyo ikiwa ni ishara na mwanzo wa kuleta maendeleao kwa wananchi wa Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakisubiria kwa muda kuanza kwa mradi huo wa ‘flyover’ ya Tazara.
Amezidi kubainisha kuwa ujenzi wa mradi huo utafanywa na mkandarasi kutoka kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction kutoka nchini Japan na utachukuwa muda wa miezi 35 kukamilka, ikifuatiwa na kipindi cha uangalizi kwa muda wa miezi 12 sawa na mwaka mmoja.
Kwa Upande wa Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida, amesema kuwa uhusiano wa Tanzani na Japan ni wa muda mrefu na kupitia mradi huu wa Flyover ya Tazara ni kielezo tosha cha kuendelea kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, utakaosaidia kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania, pamaja na kukuza uchumi wa nchi na nchi jirani.

clouds stream