Utovu wa nidhamu waendelea kumwandama Mourinho
Jose Mourinho amefunguliwa mashtaka
ya utovu wa nidhamu na Shirikisho la Soka la Uingereza kwa sababu ya
lugha aliyoitumia na vitendo vyake wakati wa mechi ambayo Chelsea
walichapwa na West Ham United wikendi.
Mourinho alifukuzwa eneo la marefa uwanjani baada yake kwenda kutaka
kuzungumza na refa Jon Moss katika chumba chake wakati wa mapumziko
mechi hiyo ya Jumamosi.Klabu zote mbili pia zimeshtakiwa kwa kushindwa kudhibiti wachezaji na zimepewa hadi Oktoba 29 kujibu mashtaka hayo.
Chelsea tayari wanakabiliwa na faini ya £25,000 kwa wachezaji zaidi ya watano kupewa kadi za manjano wakati wa mechi hiyo ya Ligi ya Premia.
Kando na kadi mbili alizoonyeshwa Nemanja Matic, Chelsea pia walishuhudia wachezaji wao Cesar Azpilicueta, Willian, Cesc Fabregas, John Mikel Obi na Diego Costa wakilishwa kadi uwanjani Upton Park.
Klabu hiyo pia itatakiwa kueleza wasimamizi wa Ligi ya Premia ni kwa nini Mourinho alikosa kuzungumza na wanahabari baada ya mechi hiyo.
Mechi hiyo ilikuwa ya tano kwa Chelsea kushindwa katika mechi 10 za ligi msimu huu na inawaacha mabingwa hao watetezi wakiwa nambari 15 na alama 11, alama 11 nyuma ya viongozi Manchester City.