Mwapachu arudisha kadi 2 CCM, atimkia kwa Lowassa
Balozi Juma Mwapachu ambaye ni mmoja kati ya wanachama wakongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM),amerudisha rasmi kadi ya chama cha Mapinduzi na ile ya TANU katika ofisi za CCM kata ya Mikocheni jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mtandao huu, Mwapachu amesema kwamba ameamua kurudisha kadi ya CCM kutokana na kutokukubaliana na uamuzi wa CCM wa kumkata mwanasiasa ambaye angeweza kuleta mabadiliko ndani ya CCM Edward Lowassa, ambaye ni Mgombea urais wa kupitia Ukawa hivisasa.
Aidha,Mwapachu ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema baada ya kurudisha kadi hizo anaungana na UKAWA ambapo mara baada ya uchaguzi mkuu ata amua ni chama gani aungane nacho.
Akizungumzia kuhusu wanaohama kutoka CCM kubezwa na kuitwa Makapi, Mwapachu amesema kwamba waliobaki CCM ndio Makapi kwa madai kuwa chama cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo na kuwa ni chama kinachotegemea maamuzi ya watu wachache.
Amesema hivisasa yeye ni Mwanaharakati, akidai kwamba mabadiliko ya msingi zaidi ni Katiba, lakini chama cha Mapinduzi toka mfumo wa vyama vingi uanze, CCM katika uongozi wake imeendelea kutojali uwepo wa vyama vingine licha ya kuwa nchi ipo katika mfumo wa vyama vingi.
Ameongeza kuwa CCM wameendelea kuhodhi madaraka na kujiona kama ni chama cha kutawala nchi hii milele yote na kwamba wakati sasa umefika kwa wananchi ambao asilimia kubwa ni vijana kuwa wanataka mabadiliko.
Katika hatua nyingine amesema amekuwa akikutana na wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu, ambao wamekuwa wakihoji kwa nini wanasiasa ndani ya chama hicho wameshindwa kuwaletea wananchi maendeleo, huku wakionekana kujinufuisha wao wenyewe ikiwa ndio msingi hasa wa mabadiliko wanayo yataka.