Saturday, 10 October 2015

Fahamu machache ya aliyekaimu nafasi ya Blatter FIFA,Hayatou

Fahamu machache ya aliyekaimu nafasi ya Blatter FIFA,Hayatou

Tarehe October 10, 2015
Issa Hayatou

Ni habari ambazo wengi wamezifurahia na hasa Afrika, lakini kiongozi wa soka barani Afrika Issa Hayatou huenda binafsi alikuwa akiogopa kutajwa kiongozi wa Fifa.
Kwa miaka 111 tangu kuanzishwa kwa Fifa, shirika hilo linalosimamia soka duniani sasa linaongozwa na Mwafrika.
Lakini Hayatou amekuwa mtu ambaye hapendi kuangaziwa sana na vyombo vya habari.
Lakini sasa, mzee huyo anayependa sana kuongoza akiwa amejifungia afisini, hataweza kukwepa wanahabari.
Kwa siku 90 zijazo, Sepp Blatter atakapokuwa amesimamishwa kazi, macho yote yatakuwa kwa raia huyo wa Cameroon na labda hata zaidi kutokana na kashfa inayokumba shirikisho hilo.
Hayatou alizaliwa kaskazini mwa Cameroon, akiwa mwana wa mmoja wa masultan wa eneo hilo. Kakake alikuwa waziri mkuu wan chi hiyo wakati mmoja.
Kama Blatter, Hayatou ni mwanasiasa mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto kwa ustadi.


Shambulio dhidi ya timu ya Togo
Wakati wa ujana wake, alikuwa mchezaji. Hayatou, 69, amekuwa makamu wa rais wa Fifa, mwanachama wa kamati tendaji ya shirikisho hilo tangu 1990, na amekuwa akiongoza soka Afrika tangu 1988.
Jinsi Caf ilivyoshughulikia shambulio lililotekelezwa dhidi ya timu ya Togo wakati wa michuano ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2010 inaashiria sifa za Hayatou.
Alikataa kufichua hatua zilizochukuliwa na Caf kushughulikia mzozo huo kwa sababu hakudhani ilikuwa muhimu kwa umma kujua hilo. Ukweli ni kwamba, aliabiri ndege usiku na kwenda hadi huko kutatua mzozo uliotokea.
Kutokana na ukosefu wa habari kuhusu hatua alizochukua, wengi walikosoa Caf wakidhani ilinyamaza.
Caf ilijibu hatua ya Togo kujiondoa kutoka kwa dimba hilo kwa kuipiga marufuku kwa miaka miwili. Uamuzi huo hata hivyo ulibatilishwa kupitia juhudi za Mahakama ya Utatuzi wa Mizozo ya Michezo na Blatter mwenyewe.
Hayatou, aliyekuwa mkurugenzi wa soka Cameroon katikati mwa miaka ya 1980 bila shaka atakabiliwa na maswali mengi atakapokutana na wanahabari mara ya kwanza.
Mitandao ya kijamii tayari imeanza kufufua madai yaliyokuwepo dhidi ya Hayatou awali, madai ambayo ameyakanusha.

Kubadilisha sheria za Caf
Moja ya haya ni kushutumiwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki 2011 kwa madai kwamba alipokea kiinua mgongo kutoka kwa kampuni ya matangazo ya michezo ya ISL kati ya 1989 na 1999.
Kwa mujibu wa IOC, Hayatou alikiri kupokea malipo hayo, akisema ilikuwa zawadi kwa shirikisho lake.
Kisha, kulikuwa na madai, yaliyosikika na wabunge wa Uingereza katika kamati ya utamaduni, vyombo vya habari na michezo ya Bunge la Commons mwaka 2011, kwamba Hayatou alipokea hongo kuhusiana na utoaji wa haki kwa Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2022, madai ambayo ameyakanusha.
Mapema mwaka huu, alisimamia kubadilishwa kwa sheria za shirikisho hilo kuhusu umri ndipo aweze kuendelea kuongoza.
Maafisa wa Caf walikuwa wakistaafu wakitimiza miaka 70, lakini hilo lilibadilishwa Aprili wanachama wote walipounga mkono kuondoa sheria hiyo.
Hii ina maana kwamba Hayatou, aliye na umri wa miaka 69 sasa, anaweza kuwania tena muhula wake ukimalizika 2017.
Sheria pia zilikuwa zimebadilishwa kupunguza nguvu za wapinzani wa Hayatou.
Caf ilipitisha sheria kwamba rais anaweza tu kutoka kwa wanachama wa kamati tendaji, ambao wengi ni washirika wa Hayatou.
Hilo lilizuia raia wa Ivory Coast Jacques Anouma kumpinga.
Lakini mashabiki wake watataja ustawi wa soka Afrika kama ishara ya utendakazi wake.
  • Alipigania kuongezwa kwa nafasi za wawakilishi wa Afrika Kombe la Dunia kutoka wawili hadi watano.
  • Alipigania kuanzishwa kwa mfumo wa mzunguko katika uenyeji wa Kombe la Dunia katika Fifa hatua ambayo mwishowe ilipelekea Afrika Kusini kuwa taifa la kwanza kuandaa Kombe la Dunia Afrika 2010.
  • Aliongeza mara dufu timu zinazoshiriki Kombe la Taifa Bingwa Afrika kutoka nane hadi 16.
  • Alianzisha shindano la vijana la chini ya umri wa miaka 20 na chini ya miaka 17.
  • Alibadilisha muundo wa Kombe la Taifa Bingwa Afrika na Ligi ya Klabu Bingwa Afrika miaka ya 1990, na pia kuanzisha ligi ya daraja la pili kwa klabu.
  • Alitekeleza dimba la bingwa wa Afrika kwa wanawake.
  • Aliimarisha sana uwezo wa kifedha wa Caf.
Hayatou, ambaye anaugua maradhi ya figo, na huhitaji kusafishwa damu mara kwa mara, kwa sasa yuko mji mkuu wa Cameroon, Yaounde na anatarajiwa kusafiri kwenda makao makuu ya Fifa mjini Zurich karibuni.
Amesema hatawania uchaguzi wa Februari lakini atasaidia kufanikisha mageuzi katika shirikisho hilo.
Alikuwa amejaribu kumng’oa Blatter katika uongozi wa Fifa uchaguzini 2002 lakini akashindwa.
Kwake, ushauri kwamba unafaa kuwa makini katika unalojitakia unafaa sana.

clouds stream