NSSF Yakiri Kuingizwa Mkenge Bilioni 270
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa linaweza kupoteza kiasi cha Sh bilioni 270, zilizoingizwa kwenye mradi wa ubia baina yake na Kampuni ya Azimio Housing Estates (AHEL), kama shirika hilo lisipokuwa makini.
Pamoja na hayo, kamati hiyo baada ya kubaini madudu kadhaa katika hesabu za shirika hilo, imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu wa mikopo yote iliyotolewa na NSSF kwa vyama vya akiba na mikopo.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mradi huo ambao ni ujenzi wa mji wa kisasa katika eneo la Dege Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara amesema kwa sasa kinachoangaliwa kwenye mkataba huo ni athari za kupoteza fedha hizo.
Profesa Kahyarara amesema pamoja na shirika hilo kuwepo kwenye ubia huo, lakini limegundua ekari zilizopo kwenye mkataba si za uhalisia.
Amesema kwa mujibu wa mkataba zilitakiwa ziwe ekari 20,000 lakini kiuhalisia baada ya kufanya tathmini zipo ekari zaidi ya 3,500.
Aidha, alifafanua kuwa bei iliyothaminiwa kwenye ekari hizo pia ni tofauti kwani mwekezaji huyo alithaminisha ardhi hiyo kwa Sh milioni 800, lakini baada ya NSSF kufanya uchunguzi wake ikabaini kuwa ekari moja thamani yake ni Sh milioni 25.
Kwa mujibu wa taarifa za CAG zinaeleza kuwa NSSF iliingia ubia na kampuni hiyo na kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Builders Limited.
Katika mkataba huo, Azimio Housing Estates itatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa kisasa wa Kigamboni kupitia mradi uliopo eneo la Dege.
Hata hivyo, mradi huo umesimama utekelezaji wake tangu Februari, mwaka huu kutokana na mwekezaji kutokuwa na fedha huku NSSF tayari ikiwa imeshaingiza Sh bilioni 270.
Katika ubia huo, NSSF inamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estates inamiliki asilimia 55 ya hisa na jumla ya gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 653.44.