RC: Watoto Wa Mitaani Wachapwe Viboko
Tarehe October 4, 2016
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amefunguka na kuamuru watoto wa kiume wenye umri mkubwa wanaoishi mitaani mjini Sumbawanga, wacharazwe viboko mahakamani ili warudi na kuishi na familia zao.
Mkuu wa mkoa huo Zelothe Steven ameamuru wazazi na walezi wa watoto hao, wasakwe popote walipo na washtakiwe kwa kuwatelekeza watoto wao na kusababisha waishi mitaani.
Zelothe alitoa maagizo hayo katika Kikao cha 30 cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC), akiunga mkono ushauri alioutoa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule.
“Hii sasa imekuwa ni kero kubwa, zipo taarifa kuwa watoto hao wana wazazi wao lakini bado wanaonekana kukizurura mitaani na kuomba omba,” amesema Zelothe.
Watoto hawa sasa wamekuwa watukutu mitaani, kwa wale wenye umri mkubwa wasakwe , wakamatwe wafikishwe mahakamani na wapewe adhabu ya kucharazwa viboko kisha warejeshwe kwa wazazi wao.
“Kwa wazazi wenye watoto hawa nao wasakwe , wakamatwe na kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wazazi wenye tabia isiyokubalika ya kuwatelekeza watoto wao na kusababisha waishi mitaani mjini hapa,” amesema Zelothe.
Naye, Dk Haule alishauri kuwa watoto 16 wanaoishi mitaani mjini humo, ambao wana umri mkubwa waliokamatwa hivi karibuni katika msako, waadhibiwe kwa kucharazwa viboko mahakamani kisha warejeshwe kwenye familia zao.
“jumla ya watoto 231 wote wavulana wamebainika kuwa wanaishi mitaani katika Mji wa Sumbawanga na umri tofauti katika msako wa hivi karibuni uliofanyika mjini hapa watoto 40 wamekamatwa na kupelekwa kuishi kwenye nyumba ya malezi ya Bethania, inayolea watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika msako huo walikamatwa watoto 16 ambao wao wana umri mkubwa nashauri wacharazwe viboko mahakamani ili waweze kurudi kwenye familia zao.