Vigogo Wa Polisi Wakamatwa Na Magari Ya Wizi
Wakazi wa Mji wa Himo, Wilayani Moshi wamelalamikia hatua ya Jeshi la Polisi kutowawajibisha maofisa wake wawili wanaohusishwa na mtandao wa wizi wa magari.
Taarifa kutoka ndani ya Polisi zinadai kuwa maofisa hao, ambao mmoja ni Mratibu wa Polisi huku mwingine akiwa Koplo walikamatwa na magari magari matatu ya wizi yaliyosafirishwa kutoka kutoka Mjini humo hadi Dar es Salaam.
Maofisa hao wanadaiwa kukamatwa na magari hayo mwezi uliopita na kikosi kazi maalum kutoka Dar es Salaam lakini hadi sasa wapo kazini.
Kukamatwa kwa maofisa hao kulitokana na kutajwa na watuhumiwa muhimu wa mtandao wa wizi wa magari Jijini Dar es Salaam waliokuwa mikononi mwa polisi ambao walisafirishwa hadi himo na kupelekea kukamatwa kwa magari hayo.
Katika operesheni hiyo, mtuhumiwa mmoja alikamatwa nyumbani kwa Koplo akiwa na gari moja la wizi na vibao 70 vya namba za magari huku ASP huyo akidaiwa kukamatwa na gari aina ya RAV4 likiwa na namba bandia huku magari mengine mawili yakikutwa kwa Koplo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alikiri vigogo hao wa polisi kukamatwa na magari hayo na kudai kuwa hawawezi kupewa adhabu hadi pale itakapothibitika kuwa wamefanya uhalifu.