Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa tuhuma nzito kuwa kuna njama za kumuua kwa kumkamata na kumpulizia sumu itakayochukua uhai wake taratibu.
Seif aliyezaliwa Oktoba 22, 1943 katika Kijiji cha Nyali Wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba ameyasema hayo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Baraza Kuu, Viongozi, Watendaji na Wafuasi wa CUF alipokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo ametimiza miaka 73.
Bila kutaja wanaotaka kumuua, amesema kuwa kuna taarifa za kuaminika kwamba zipo njama za kumkamata na kupelekwa Dar es Salaam kama walivyofanyiwa masheikh, waniweke kwenye chumba maalum kidogo kasha wanipulizie dawa ili afya yangu izorote polepole na mwisho nifariki dunia.
Amesema hujuma za kutaka kumuua zipo tangu zamani lakini ni Mwenyezi Mungu ndiye ameweza kumlinda, hivyo hajali wala kuogopa chochote.
Kiongozi huyo ambaye alikuwa pia Makamu wa Kwanza wa Rais kwa iliyokuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) amesema kuwa kama ana makosa yoyote ni vyema sharia ikachukua mkondo wake kwa kumfikisha mahakamani.
Akizungumzia tuhuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Abood Mohamed amesema Serikali itatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
“Waulizeni Jeshi la Polisi wanaweza kuwapa taarifa , lakini kwa upande wa Serikali ya Zanzibar itatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo,” amesema.
Naye Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Hamdan Onar Makame amesema hana taarifa zozote kuhusiana na suala hilo.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Salum Msangi pia amedai kutokuwa na taarifa za Maalim Seif kuzungumza maneno hayo lakini akaahidi kuzifanyia kazi ili kufahamu ukweli wa maneno hayo.