Mashabiki Yanga Wamlilia Pluijm
Siku moja baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm, kuandika barua ya kujiuzulu kuwafundisha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kundi la mashabiki wa timu hiyo wameonesha kutoridhishwa na uamuzi huo na kuutupia lawama uongozi kwa kusababisha kuondoka kwa mpendwa wao huyo.
Pluijm ameifundisha timu hiyo kwa misimu miwili na kuipa mafanikio makubwa ikiwemo kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu hatua ambayo ilikuwa haijafikiwa na timu hiyo kwa kipindi cha miaka 18 nyuma.
Baadhi ya mashabiki wamesema hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi wao wa juu na wengine kudai hawatoona ajabu kwa timu hiyo kushindwa kutetea ubingwa wake kutokana na kubadilisha kocha wakati ligi ikiendelea.
Hamisi Abdallah mwanachama wa Yanga kutoka tawi la Buguruni, amesema, binafsi angependa Kocha Pluijm aendelee kuifundisha timu hiyo kwa sababu bado hajaona mabaya aliyoyafanya na hasa ukizingatia mafanikio aliyowapa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Abdallah amesema, kama uongozi ulitaka kumbadilisha kocha huyo ungesubiri wakati wa dirisha dogo na siyo kipindi hiki, ambacho ligi ipo kwenye ushindani na wapinzani wao Simba wameonekana kujipanga kuwapoka ubingwa wao.
Naye Emmanuel Mgamilo, shabiki wa Yanga kutoka Magomeni amesema, kitendo wanachokifanya viongozi wa Yanga kinaweza kuitafuna timu hiyo kushindwa kupata taji lolote msimu huu, kwani kumbadilisha Kocha Pluijm na kuleta kocha mpya ni sawa na kuwachanganya wachezaji.
Mgamilo, alisema kwa mafanikio ambayo wameyapata chini ya Pluijm kocha huyo alikuwa na nafasi ya kuendelea kuifundisha timu hiyo na sababu ambazo uongozi wao umezichukua hata kumtimua kocha huyo hazina mashiko kwani ni sawa na kumdhalilisha kwani rekodi zake zinajieleza wazi.
Kocha Pluijm aliamua kuandika barua ya kuacha kazi muda mfupi baada ya kupata taarifa ya kuwasili Kocha wa Zesco United, Mzambia George Lwandamina, ambaye kwa muda wa wiki sasa taarifa zake zilizagaa nchini kuja nchini kuziba nafasi ya Mdachi huyo ambaye alitua Yanga kwa mara ya kwanza mzunguko wa pili wa msimu wa 2013/14 akichukua mikoba ya Mholanzi mwenzake Ernie Brandts na aliweza kumaliza nafasi ya pili nyuma ya waliokuwa mabingwa wa msimu huo Azam.
Kabla ya msimu wa 2014/15 kuanza kocha huyo aliomba kuvunja mkataba wake na kuondoka baada ya kupata timu ya kufundisha nchini Saudi Arabia ‘Al Shaola FC’ na alimchukua aliyekuwa msaidizi wake Boniface Mkwasa, lakini hawakudumu sana alitimuliwa huko na kuamua kurudi Ghana anapoishi wakati huo Yanga ikimchukua Mbrazil Marcio Maximo aliyeziba nafasi yake lakini baada ya uongozi wa Yanga kutoridhishwa na mwenendo wa timu yao kwenye ligi uliamua kuachana na Maximo karibu na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza.
Msimu uliofuata wa 2015/16 Pluijm aliiwezesha Yanga kutetea ubingwa huo akiwa ameanza nayo mwanzo na kusajili yeye nyota kadhaa akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Hajji Mwinyi na nyota wengi ambapo mbali na kutetea ubingwa pia walibeba Kombe la FA lililofanyika kwa mara ya kwanza baada ya kusimama kwa muda na pia aliweza kuifikisha timu hiyo raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa kwa mabao 21 na Al Ahly ya Msri na kuangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambapo walifanikiwa kutinga hatua ya makundi.
Pluijm mwenyewe amesema kilichomfanya aandike barua ya kujiuzulu ni dharau aliyooneshwa na viongozi wa Yanga kwa kumleta nchini kocha mpya bila kumtaarifu yeye na amewaomba radhi mashabiki na wanachama wa timu hiyo.