Saturday 22 October 2016

Shein: Hatutoi Mikopo Wanafunzi Elimu Ya Juu.

shein
V 2

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kusimamisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, hadi hapo serikali itakapojiridhisha na utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo hiyo.

“Hatutatoa mikopo mwaka huu mpaka hapo tutakapokamilisha kazi ambayo tumeanza kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo ili kuhakikisha inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa wanaostahili,” amesema Dkt. Shein.

Akizungumza katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne mwaka 2015 na Kidato cha Sita mwaka 2016, Dkt. Shein amesema kuwa katika utaratibu wa sasa wapo waliodanganya kupata mikopo na ambao wamekopeshwa lakini wamekuwa wagumu kurejesha mikopo hiyo.

Katika hafla hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na wengine 50 waliomaliza kidato cha sita, walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza katika mitihani yao ya taifa.

“Wako waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo mko 50 wa kidato cha tano mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la kwanza mtihani wa kidato cha nne,” amesema Dkt. Shein na kuhoji msingi wa kukebehi matokeo hayo.

clouds stream