Sunday 30 October 2016

Bodi Yafafanua Vigezo Vya Mikopo Na Waliokosa Mikopo Elimu Ya Juu

1
V 2

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi kuhusu vigezo inavyotumia katika kuchambua, kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 (asilimia 74) wa mwaka wa kwanza hadi sasa kati ya 25,717 iliyopanga kuwapa mikopo katika mwaka huu wa masomo, 2016/2017.

Idadi iliyobaki (asilimia 26) ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza itajazwa na waombaji ambao baadhi ya nyaraka walizowasilisha zinaendelea kuchambuliwa ili kuthibitisha uhalisi wake na baadhi zitajazwa na waombaji ambao wanakata rufaa na kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya mwaka huu.

Aidha, katika mwaka huu wa masomo, Serikali imepanga kutumia jumla ya Tshs 483 kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na 25,717 wa mwaka wa kwanza.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana (Jumapili, Oktoba 30, 2016), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul­Razaq Badru alisema vigezo vikuu vinavyotumika mwongozo uliotangazwa na Bodi hiyo wakati ilipotangaza kuanza kupokea maombi mwezi Juni mwaka huu ambao unataja makundi makuu matatu ya watakaopata mikopo.

Vigezo vilivyotumika kutoa mikopo

Kwa mujibu wa Bw. Badru, kundi la kwanza linajumuisha wanafunzi waombaji wa mikopo wenye uhitaji maalum kama wenye ulemavu uliothibitishwa na Waganga Wakuu wa Wilaya na yatima ambao katika maombi yao waliwasilisha nakala za vyeti vya vifo zilizothibitishwa na makamishna wa viapo.

“Kundi la pili linajumuisha waombaji wa mikopo ambao baada ya uchambuzi wa taarifa zao walizowasilisha na baada ya kulinganisha na gharama za jumla za masomo yao ya sekondari, wamebainika kuwa wana uwezo mdogo wa kugharamia masomo yao ya elimu ya juu na hivyo kuwa na uhitaji zaidi wa mikopo,” amesema Bw. Badru.

Badru ametaja kundi la tatu na la mwisho kuwa linajumuisha waombaji wa mikopo ambao wenye ufaulu wa juu katika matokeo yao ya kidato cha sita na wamechaguliwa kujiunga na fani za kipaumbele kwa taifa.

Fani hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, uhandisi wa Kilimo, Mafuta na Gesi na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.

Makundi ya wanafunzi waliopata mikopo

“Hivyo basi, hadi sasa tumetoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 wakiwemo wanafunzi yatima 4,321, wenye ulemavu 118, wanafunzi wenye uhitaji waliosomeshwa na taasisi mbalimbali katika masomo ya sekondari (87), wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na wanafunzi wanaosoma kozi zisizo za kipaumbele lakini wanaotoka kwenye familia duni 9,498,” amefafanua Bw. Badru.

Sababu za kukosa mikopo

Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa HESLB pia ameeleza kwa kina sababu nyingine za waombaji 27,053 ambao hawajapangiwa mikopo.

Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya waombaji (90) kuwa na umri wa zaidi ya miaka 30, waombaji mikopo waliopata udahili kwa sifa linganishi (equivalent qualifications) na waombaji waliomaliza masomo ya kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Kundi jingine la waombaji waliokosa mikopo katika awamu ya kwanza ni waombaji waliopata nafasi katika vyuo kwa ufaulu wa mitihani waliyofanya kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) na waombaji ambao hawakurekebisha fomu zao za maombi ingawa waliitwa kufanya hivyo.

Nafasi ya rufaa na uhakiki wa wanafunzi wanaoendelea na masomo

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amewataka waombaji ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo unaotangazwa, kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa kuanzia katikati ya wiki hii.

“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa mkopo kwa kutowasilisha baadhi ya nyaraka ingawa tuliwaomba kufanya hivyo, hawa na wengine wenye sababu za msingi, watapata fursa ya kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao na nakala kuzituma kwa utaratibu tutakaoutangaza wiki inayoanza kesho(leo),” amesema Bw. Badru.

Aidha, Bw. Badru amesema bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kazi kuhakiki taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wanapata mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kubaini kama ni wana uhitaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa vigezo au hapana.

Katika zoezi hili linalotarajiwa kufanyika kwa siku 30 kuanzia mwezi ujao (Novemba, 2016), wanafunzi wote ambao ni wanufaika watalazimika kujaza dodoso maalum litakalokusanya tarifa za kiuchumi za wazazi na walezi wao ili kuweza kupata uhalisia wa sasa.

“Wanafunzi watakutana na dodoso katika akaunti zao katika mtandao wetu wa maombi ya mikopo (OLAMS) na watapaswa kujaza. Wale ambao hawatajaza dodoso hili kwa njia ya mtandao tutasitisha mikopo yao na wale ambao baada ya uchambuzi tutabaini hawana uhitaji, nao tutasitisha mikopo yao na watapaswa kuanza kurejesha fedha walizokopokea,’ amefafanua.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.

clouds stream