Thursday, 13 October 2016

Simba, Yanga Na Stand United Zang’ara VPL

Tarehe October 13, 2016
Image result for vpl tanzania 2016/17V 2

Mambo yameonekana kuzinyookea Timu za Simba, Yanga na Stand United jana baada ya timu hizo kushinda mechi zake za Ligi Kuu zilizochezwa kwenye viwanja tofauti.

Vinara wa ligi hiyo, Simba wakiwa ugenini Mbeya walichomoza na ushindi wa mabao 2­0 dhidi ya Mbeya City katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Sokoine mjini humo. Ambapo ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kujikita kileleni ikiwa na pointi 20 katika mechi zake nane ilizocheza.

Mashujaa wa Simba jana walikuwa Ibrahim Ajib aliyefunga bao la kuongoza katika dakika ya 6, baada ya kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja golini na Shizza Kichuya aliyefunga bao la pili katika dakika ya 33 ya mchezo baada ya kuwachambua mabeki wa Mbeya City ambao walionekana kupwaya tangu mwanzo wa mchezo.

Nao mabingwa watetezi Yanga FC walichomoza na ushindi wa mabao 3­1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 14 na kusogea hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi saba.

Mabao ya Yanga jana yalifungwa na Obrey Chirwa katika dakika ya 45 akiunganisha mpira wa Simon Msuva na kuujaza mpira wavuni huku bao la pili likifungwa na Saimon Msuva katika dakika ya 68, huku Donald Ngoma akikamilisha Ushindi wa magoli 3 kwa kuiongeza Yanga bao la tatu katika dakika ya 79.

Kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga, Stand United iliendelea kushangaza mashabiki wa soka baada ya kuifunga Azam bao 1­0, Ushindi unaoifanya Stand kuendelea kukaa kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19 katika mechi tisa ilizocheza.

Nako CCM Kirumba Mwanza, Toto Africans ilikubali kipigo cha mabao 3­1 kutoka kwa timu ngeni kwenye ligi Mbao FC ambapo Mbao FC iliata bao la kuongoza katika dakika ya 39 kupitia kwa Dickson Ambundo kabla Waziri Junior hajaisawazishia Toto katika dakika ya 41.

Mbao ilianza kipindi cha pili kwa kasi na katika dakika ya 58 Hussein Swedi aliiandikia bao la pili kabla Boniface Maganga hajaongeza bao la tatu katika dakika ya 90.

Mechi nyingine ilichezwa jana kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi ambapo wenyeji JKT Ruvu walitoka suluhu na Prisons.

clouds stream