Wednesday 26 October 2016

Asilimia 90 Wanafunzi Elimu Ya Juu Kupata Mikopo Kesho

kassim3
V 2
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia kesho asilimia 90 ya wanufaika mikopo ya elimu ya juu watakuwa wameshapata fedha zao.
Maliwa ameyasema hayo jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kudai kuwa kwa taarifa aliyonayo aliyoipata jana asubuhi wachache sana walikwishaanza kulipwa tangu juzi na kuwa ulipaji huo utaendelea hadi siku ya kesho ambapo asilimia 90 ya wanaopaswa kulipwa watakuwa wamepata fedha hizo.
“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi wa malipo ya fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo taarifa lazima zitolewe haraka ili kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na Serikali yao,” amesema.
Wakati huohuo Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivisasa.
Amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).
Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
“Ninatambua kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post­Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu nyingine, hali hii inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70,” amesema.

clouds stream