Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Guinea Bissau
Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Guinea Bissau, Jose Mario Vaz mgombea wa chama cha PAIGC ameshinda uchaguzi huo. Mario Vaz amemshinda mgombea wa kujitegemea Nuno Gomes Nabiam kwa kupata karibu asilimia 62 ya kura. Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kujiri mapinduzi ya kijeshi miaka miwili iliyopita yaliyopelekea kuanza kipindi cha mpito. Miaka miwili iliyopita Jenerali Antonio Indjai kwa kutumia mapinduzi ya kijeshi aliingia madarakani lakini kutokana na mashinikizo ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS alikubali kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito.
Ijapokuwa kwa mujibu wa maafikiano kati ya Jenerali Antonio Indjai na wapatanishi wa ECOWAS uchaguzi ulitakiwa ufanyike ili kukabidhi madaraka, lakini baadhi ya duru zimetilia shaka iwapo Jose Mario Vaz rais mtarajiwa ataweza kuwakinaisha wananchi wa Guinea Bissau. Katika nchi hiyo koloni la zamani la Ureno iliyopata uhuru mwaka 1974, hadi sasa hakuna rais aliyechaguliwa na wananchi na kuweza kumaliza kipindi chake cha uongozi. Hii ni kwa sababu mapinduzi kadhaa ya kijeshi na uasi wa mara kwa mara wa wanaejshi umekuwa ukisababisha vurugu na machafuko nchini humo. Hivi sasa pia kwa kuwa serikali ya mpito katika miaka miwili iliyopita imekuwa ikiungwa mkono na majenerali wa jeshi, hii inaonesha kuwa bado wanajeshi wana satwa na ushawishi katika siasa na uongozi wa nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, tangu Guinea Bissau ipate uhuru hadi sasa kumekuwepo na mashindano ya kudumu kati ya serikali zinazoingia madarakani na jeshi la nchi hiyo. Mashindano hayo yaliyosababisha umwagaji damu sambamba na mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara, vimepelekea nchi hiyo kukosa utulivu, ambapo majenerali wengi wa kijeshi wametumia hali hiyo kujinufaisha kwa kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya. Hali hiyo imeigeuza Guinea Bissau iliyoko Magharibi mwa Afrika kuwa kituo cha kusafirishia dawa za kulevya kutoka Amerika ya Latini kuelekea bara la Ulaya.
Kwa ajili hiyo iwapo Gomes Nabiam atadai kuwepo udanganyifu katika uchaguzi na kushitaki katika mahakama kuu ya Guinea Bissau, kuna uwezekano wa kutokea vurugu kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili. Nabiam mgombea aliyeshinda ana muda wa masaa 48 kushitaki katika mahakama kuu ya nchi hiyo, ambayo ina uwezo wa kubadilisha matokeo ya uchaguzi.
Wachambuzi wa mambo wanasema, kwa kuwa rais ajaye wa Guinea Bissau atapaswa kukabiliana na migogoro ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, pengine mgombea atakayeshindwa hatotaka kulalamikia matokeo ya uchaguzi. Hali mbaya ya kiuchumi ya Guinea Bissau imeshadidi kiasi kwamba José Ramos-Horta Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mariadhiano na Amani nchini Guinea Bissau ametaka jamii ya kimataifa iwasaidie wananchi na serikali ya nchi hiyo. Ramos-Horta ametahadharisha kuwa, iwapo utawala wa katiba hautohuishwa haraka huko Guinea Bissau, kuna uwezekano wa uchumi wa nchi hiyo kusambaratika.