Kigwangalla awataka Wazee wawapishe vijana Urais 2015
Mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora Dk,Hamisi Kigwangalla amewataka wazee wakae pembeni na kusistiza kuwa huu ni wakati wa vijana kuliongoza taifa hili na ameahidi kuwa iwapo atapitishwa na chama chake na akashinda atahakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya.
Akihutubia wananchi wa Jimbo la Nzega mjini Nzega, Dk Kigwangalla alisema wengine wote waliobaki sio wazoefu wa kufanya kazi Ikulu bali ni wazoefu wa shughuli nyingine.
Amesema ni wakati wa watu ambao hawajaingia serikali kushika wadhifa wa urais kwani uzoefu umeonesha kuwa marais ambao huwa wameshafanya kazi serikalini huwa wanaharibiwa na mfumo na hivyo kutofanya vizuri. “Umefika wakati wa kuwa na rais ambaye hajafanya kazi serikalini, wazee watupishe sasa ni wakati wa sisi vijana,” alisema Dk Kigwangala.
Hakuna uzoefu katika nafasi ya urais bali wenye uzoefu huo wapo wanne ambao tayari wamekwisha pitia nafasi hiyo na kukaa kwenye jengo la Ikulu ambao aliwataja kuwa Baba wa Taifa Mwl, Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Rais Jakaya kikwete.
Amesema kuwa wote wanaowania nafasi hiyo akiwepo yeye mwenyewe wanauzoefu tofauti tofauti katika masuala mbalimbali, huku akiwabeza wenye uzoefu wa ubadhilifu wa mali za umma ikiwemo Rushwa na ufisadi hali ambayo akiteuliwa na kushinda nafasi hiyo atapambana navyo.
Akizungumzia vipaumbele vyake amesema atahakikisha ndani ya mwaka mmoja, Watanzania wote watakuwa na Bima ya Afya watakao lipiwa na Serikali pamoja na kuwajari watumishi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili waweze kutoa huduma bora ya matibabu kwa wananchi.
Amesema katika kuboresha suala la Elimu kwa watanzania kama atashika nafasi hiyo anatamanai Elimu yote kuanzia Awari,msingi na sekondari bure kwa kuwa atahakikisha nchi inakuwa na uchumi imara kwa kupunguza matumizi ya serikali,safari,posho na ukubwa serikali.
Kwa upande wa kukuza uchumi kwa wakulima, wafanya Biashara wadogowadogo na viwanda anatamani kuanzisha mfuko wa kukopesha wananchi kwa kuwekeza Bill 500 kwa mwaka pamoja na kuboresha kitengo cha ustawi wa jamii katika Halmashauri kwa ajili ya kuelimisha,kuwaunganisha kwenye vikundi vya kudhaminiana na kuratibu shughugili zao.