Urais 2015: Mwandosya ‘amtisha’ lowassa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya amemtaka Mbunge wa Monduli Edward Lowassa asisite kumuunga mkono kama walivyofanya watangaza nia wengine ili mambo yaishe mapema.
Mwandosya alisema hayo mwishoni mwa wiki wilayani Mbozi alipokuwa akizungumza na wanaCCM waliomdhamini katika mbio zake za urais, pamoja na wanachama wengine waliojitokeza katika Ofisi za CCM.
Nimesikia Membe amesema hapa Mbeya asipopitishwa yeye basi atamuunga mkono Profesa Mwandosya, nikasikia tena na Waziri Mkuu akisema hata kama asipopitishwa yeye atafarijika kama Profesa Mwandosya atakuwa mgombea, nikasikia tena na Wassira naye kupitia kwa mtu wake wa karibu ataniunga mkono, sasa namuomba mwenzangu naye Edward au maarufu kama Edo naye aseme Profesa ndiyo wangu, ili kazi iishe na tuipunguzie kazi Halmashauri Kuu,” alisema Profesa
Katika mkutano huo alisema amefarijika kusikia anaungwa mkono na wagombea wenzake ambao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe pamoja na kupata taarifa za Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira naye kusema anamuunga mkono.
Kufuatia kuungwa mkono na watangaza nia hao watatu anamuomba pia Lowassa naye kumuunga mkono ili kuipunguzia kazi Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM).