Museveni apata mpinzani wa kipekee
Rais Yoweri Museveni amekuwa madarakani kwa karibu miaka 30 toka alipotwaa madaraka mwaka 1986. Katika kipindi hiki chote amekumbana na wapinzani wa aina tofauti tafouti.Amekumbana na wapinzani wa kijeshi (waasi), amekumbana na upinzani ndani ya chama na serikali yake na wale wa siasa wa vyama vya upinzani.
Mmoja wa wapinzani ambao amekumbana nao na ambao wameonekana kumuhenyesha kweli ni yule aliyekuwa mtu wake wa karibu sana kiasi cha kuwa daktari wake walipokuwa wakipagania madaraka, Kanali Mstaafu Kizza Besigye.
Baada ya Museveni kutwaa madaraka, Besigye alikuwa mmoja wa kundi lililokuwa na madaraka katika jeshi na kwenye duru za Utawala.
Lakini mwaka 2001 Besigye alitangaza kumpinga Museveni upinzani ambao hadi sasa pande zote, waganda na Ulimwengu unaukumbuka. Kwa mara mbili mfululizo, mwaka 2006 na 2011 pande hizo mbili zilimenyana katika uchaguzi mkuu, na mara zote Besigye akitangaza kuwa alikuwa ameshinda isipokuwa Museveni aliiba kura.
Katika vinyanganyiro hivyo kulijitokeza sura ya serikali kutumia nguvu sana kumdhibiti Besigye na wakati mmoja Besigye ‘alikimbilia’ uhamishoni nje ya Uganda akirudi baada ya muda. Besigye amekamatwa mara kadha na kuswekwa ndani; moja ya operesheni za kumkamata zinazokumbukwa mno ni ile yeye na abiria waliokuwa kwenye gari lake walipomwagiwa pilipili kwenye gari yake na akaburuzwa hadi kwenye gari la wanausalama, vitendo vilivopelekea akimbizwe hospitali Nairobi kwa matibabu.
Wapinzani na wapenzi wa Museveni wote wameongezeka toka mwaka 2001, lakini hapajawepo mpinzani mwenye nguvu na ushawishi ndani ya chama chake kama, Bw. Amama Mbabazi, mwanasiasa mkongwe na swaiba wa Museveni kwa miaka mingi akishika nyadhifa tofauti Serikalini mara ya mwisho akiwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa Chama tawala cha Museveni cha NRM.
Bw Mbabazi ni tofauti kwa sababu amejitokeza hadharani na kutangaza kuwa atachuana na Museveni kukiwakilisha chama chao kama Mgombea wa Urais, huku kamati ya chama hicho ikiwa tayari imeshatangaza kuwa Museveni hatokuwa na mpinzani kwenye chama hicho.
Ni takribani miezi 8 sasa toka Mbabazi ayenguliwe kutoka kwenye nyadhifa yake ya Waziri Mkuu, kuenguliwa kuliosemekana kutokana na ‘njama za wazi’ za kutaka na kujipanga kuwa Rais wa Uganda.
Katika kipindi hicho chote, kumekuwepo na sauti za chini chini kuwa Mbabazi angeligombea Urais lakini yeye mwenyewe alikuwa hajasema wazi wazi. Lakini sasa kaweka bayana kuwa atachuana na Museveni kwanza ndani ya chama, na akiibuka kidedea atagombea Urais wa nchi ya Uganda.
Makamanda wawili wameshavaa magwanda, maswali matano muhimu ni je,
1. nani ataibuka kidedea?
2.Nini hatma ya atakayepoteza katika hawa wawili?
3. Nini hatma ya chama cha NRM?
4. Museveni, anayesifika kwa mbinu za kisiasa na vita, ataweza kuvuka kwenye uchaguzi 2016?
5. Je baada ya miaka 30 ya Museveni, Uganda imekomaa kiusalama, kidomkrasia na utawala kuweza kuhimili mitikisiko ya sasa?