Meli yazama nchini China, abiria 400 hawajulikani walipo
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali Xinhua watu wanane wameokolewa mpaka sasa na kazi inaendelea ya kuwaokoa abiria wengine.
Waziri Mkuu Li Keqiang anaelekea katika eneo la tukio hivisasa kuangalia namna ya kuwaokoa abiria waliokuwa wanasafiri katika meli hiyo huku kazi ya uokoaji imekwamishwa na upepo mkali na mvua kubwa. Meli hiyo ilizama katika kaunti ya Jianli katika jimbo la Hubei.
Meli hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mashariki mwa mji wa Nanjing kwenda Chongqing kusini magharibi ilipozama. Meli hiyo, Dongfangzhixing au Nyota ya Mashariki ilikuwa imewabeba abiria wa Kichina 405, wafanyakazi watano wa shirika la usafiri na wafanyakazi 47 wa meli hiyo.
Nahodha na mhandisi mkuu, ambao ni miongoni mwa waliokolewa wamekaririwa wakisema kuwa meli ilikumbwa na kimbunga na kuzama haraka. Waliokuwa katika meli hiyo wengi wao walikuwa watalii wenye umri kati ya miaka 50 na 80 wakiwa katika safari ya kitalii iliyokuwa imeandaliwa na kampuni ya Shanghai.
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la serikali ya China, meli hiyo inamilikiwa na Shirika la Meli la Chongqing Eastern ambalo linaendesha shughuli za utalii katika maeneo matatu ya vivutio katika mto Yangtze.