Tarehe August 31, 2016
Aliyekuwa Katibu wa Chadema, Mkoa wa Mwanza, John Nzwalile
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo baada ya Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza, John Nzwalile kujivua nyadhifa zake tatu alizokuwa akizishikilia ikiwa ni pamoja na uanachama kwa madai kuwa chama hicho kimekuwa na ubabaishaji.
Nzwalile ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu CHADEMA, amesema chama hicho kimekuwa kikiwachonganisha wananchi na Serikali yao jambo ambalo halikubaliki.
“Nimefikia uamuzi huu mgumu wa kujivua nyadhifa zangu zote na uanachama wa Chadema baada ya kuchoshwa na siasa za uchochezi, majungu na uchonganishi zinazofanywa na chama hiki kikubwa cha upinzani nchini,” amekaririwa akisema Nzwalile.
Ameongeza kuwa amechoshwa na siasa hizo baada ya kuona kila mara viongozi wa Chadema wakijifungia ndani kwenye vikao vyake ni kuhusu maandamano na uchochezi tu, “kwanini tusifanye shughuli za maendeleo badala ya kuhamasisha vurugu na uvunjifu wa amani,” amehoji.
Kada huyo anajivua uanachama ikiwa imebaki siku moja tu kuanza kwa ‘operesheni’ Ukuta iliyoandaliwa na Chadema.