Maalim Seif Awekwa Mtu Kati Kuhusiana Na Tuhuma Za Ufisadi
Tarehe August 11, 2016
Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imemhoji Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia kuhusishwa kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tuhuma za ufisadi.
Afisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma cha ZAECA, Abubakari Mohamed Lunda, amesema kuwa Maalim Seif alihojiwa na Mkurugenzi wa ZAEC, Mussa Haji Ali, ili athibitishe tuhuma hizo nzito zilizotolewa dhidi ya watendaji na viongozi na kupelekea mamlaka hiyo kuamua kuchunguza ukweli wake kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
Amesema kazi kubwa ya mamlaka hiyo ni kuchunguza jambo lolote ambalo linahusu maslahi ya Zanzibar katika kupambana na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi na nia ya kumhoji Maalim Seif ilikuwa kupata ukweli wa tuhuma alizotoa dhidi ya viongozi na watendaji aliowatuhumu kwa kumiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.
“Tayari mamlaka imemhoji Maalim Seif ili kutafuta ukweli juu ya tuhuma alizotoa za kuwapo viongozi wanaomiliki fedha chafu na mali nje ya nchi,” ameongeza.
Hata hivyo, Lunda amesema mpaka sasa hafahamu mkurugenzi amegundua kitu gani baada ya kufanyika kwa mahojiano hayo huku akisisitiza kuwa ZAECA imetimiza wajibu wake wa kupokea na kuchunguza taarifa mbalimbali wanazopata kupitia wanasiasa, vyombo vya habari na wananchi ambapo tayari kuna majalada 20 yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee kwa ajili ya hatua za kisheria kuchukuliwa.
Amesema majalada hayo yanahusisha kesi mbalimbali zikiwamo za rushwa ya uchaguzi zilizotokea wakati wa kura ya maoni ya kuwapata wagombea wa ubunge na uwakilishi kupitia CCM mwaka jana.
Naye Maalim Seif, ambaye ni alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar alituhumu baadhi ya viongozi na watendaji wa visiwani humo kumiliki fedha chafu na mali nje ya nchi.
Amesema fedha hizo zilipatikana kwa njia za ufisadi na kutaka jumuiya ya kimataifa kufuatilia akaunti za vigogo hao na watendaji nje ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake na kuongeza kuwa haihitajiki tochi kuwamulika viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi na kutaka mamlaka za dola kufanya uchunguzi dhidi ya vigogo hao na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.