Tarehe August 11, 2016 8/11/2016
Hatimaye Jeshi la Polisi limefanikiwa kumtia nguvuni tabibu maarufu wa tiba asilia, Dokta Mwaka maarufu kama Dokta JJ Mwaka kufuatia agizo la Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla.
Dokta Mwaka ambaye alikuwa anatafutwa na polisi tangu juzi aliweza kujisalimisha polisi jana na kushikiliwa kwa mahojiano zaidi baina yake na Jeshi la Polisi.
Tabibu huyo wa Tiba Mbadala kutoka Foreplan Clinic alikuwa akisakwa na polisi kwa kile kilichodaiwa kukaidi uamuzi wa Serikali wa kufutia usajili kituo chake na badala yake akaendelea kutoa huduma hizo kama kawaida.
Hivi karibuni Dokta Mwaka alikuwa miongoni mwa matabibu wa tiba mbadala waliofutiwa usajili huku wengine wakisimamishwa kwa muda na tayari baadhi yao wamekwishakimbilia mahakamani ili kupewa ruhusa ya kufungua kesi dhidi ya Serikali kufuatia uamuzi wa kuwafutia leseni zao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamdani alisema jana kuwa baada ya kujisalimisha muda huo, alihojiwa na kuachiwa kwa dhamana lakini akatakiwa kuripoti leo kwa mahojiano zaidi.
“Kuhusu kupelekwa mahakamani, ni mpaka jeshi la Polisi litakapomaliza kukusanya ushahidi na kumkabidhi DPP ambaye atautumia kufungua kesi,” amesema.