Monday, 29 August 2016

Waumini Waingia Na Mabango Kanisani Kumpinga Askofu

Tarehe August 29, 2016
DSCN0546V 1

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki, Kanisa Kuu la Mtwara wameingia katiba ibada na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali za kumpinga Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Lucas Mbedule kwa tuhuma za kukiuka Katiba, Unyanyasaji wa watumishi na ubadhirifu wa fedha za Ushirika wa Dayosisi hiyo.

Pamoja na mabago hayo, Umoja wa Wazee katika Kanisa hilo ulitoa tamko ndani ya kanisa hilo kutokana na tuhuma zinazomkabili askofu huyo huku wakimtaka asijihusishe na mambo yanayohusu usharika wa dayosisi hiyo ili kuweza kupisha uchunguzi.

Wazee hao wamemuomba Askofu Mkuu wa KKKT, Dkt. Fredrick Shoo aunde tume itakayoweza kuchunguza tuhuma hizo.

Akisoma tamko la Wazee hao ndani ya Kanisa, Amon Mkocha amesema kuwa wanapinga uamuzi uliofanywa na kikao cha halmashauri kuu huku akidai ukiukwaji wa katiba uliofanyika ni pamoja na kumsimamisha msaidizi wa Askofu, Yeriko Ngwema na kumpangia kuwa mchungaji wa Ushirika wa Kilwa Masoko ambako hakuna jengo la kuabudia huku akitakiwa kukabidhi ofisi maramoja.

“Kwa kuwa mojawapo ya wajibu wa Mzee wa Kanisa kama ilivyotajwa katika Kanuni ya Katiba, Dayosisi ya Kusini Mashariki, inatutaka kuhakikisha kanuni, sheria na miongozo ya dayosisi inafuatwa na Wakristo na ndiyo maana tumelazimika kupinga uamuzi huo,” amesema.

Wazee hao pia wamedai kuwa kumekuwa na ukiukwaji wa taratibu za ajira kwa watumishi wa kanisa hil kutopewa taarifa zinazohusu maslahi yao kama zinavyotajwa kwenye sheria ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa mishahara.

Naye Mtuhumiwa, Askofu Mbedule alipotafutwa kwa njia ya simu alidai kuwa asingependa kuyazungumzia kwa sababu walikaa kikao.

“Kimsingi tulikaa katika kikao, kwa hiyo nisingependa kulisemea sana. Nilifuata taratibu za kikao,” amesema.

clouds stream