Tarehe August 4, 2016
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala.
Operesheni ya UKUTA iliyojipatia umaarufu mkubwa hivisasa inayoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imeendelea kukutana vigingi kufuatia mkuu wa mkoa wa Mbeya , Amos Makalla kupiga marufuku.
Makalla alieleza msimamo wa mkoa wake kuhusiana na operesheni hiyo katika kikao cha kazi kilichoshirikisha kamati ya ulinzi na usalama mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, ambapo alitangaza kupiga marufuku mkutano wowote utakaofanyika chini ya utaratibu unaoitwa Operesheni Ukuta.
Licha ya kupiga marufuku operesheni hiyo Makalla alisema wabunge na madiwani akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) wa Chadema wanaweza kufanya mikutano yao bila wasiwasi katika maeneo yao.
Makalla amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi vimewekwa tayari kuwashughulikia kwa nguvu zote watakaokaidi maagizo yanayotolewa na kutoa wito kwa vijana wa mkoa huo kuwafichua watu wenye njama zozote zikiwamo za kuwahamasisha kufanya maandamano.
Makalla anakuwa mkuu wa mkoa wa pili kupiga marufuku Maandamano hayo mara baada ya mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi naye kutangaza kupiga marufuku maandamano hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika septemba 1 nchini nzima.