Mrema Awaonya Tena Chadema, Maandamano Ya UKUTA
Tarehe August 13, 2016
Mwenyekiti wa chama cha TLP Auguustino Mrema. Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustino Mrema amewaonya Viongozi pamoja na wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuachana na maandamano ya Ukuta ifikapo septemba 1,mwaka huu.
Akizungumza kwenye mahojiano na moja ya kituo cha redio hapa nchini Mrema alisema wapinzani wanatakiwa kufanya siasa kama anayoifanya yeye ya kuwa mpinzani mstaarabu ambaye anaunga mkono kazi zinazofanywa na Rais Magufuli. “Mimi ni mpinzani mstaarabu, upinzani wa kijinga siutaki kama wewe ni mpinzani wa kweli inatakiwa ukae bungeni ili kutoa matatizo ya watanzania lakini sasa wao wanatoka, niwashauri tu wakae wafanye kazi,” alisema Mrema.
Mrema amewataka wanachama wa Chadema na Ukawa kuacha maandamano hayo na badala yake waende shambani kulima au kusaidia kutatua tatizo la madawati kama wamekosa kazi ya kufanya.
Chama cha Chadema hivi karibuni kimetangaza tarehe 1septemba kuwa ni siku ya kufanya mikutano kisiasa hapa nchini kwa madai ya kuchoshwa na utawala wa awamu ya tano uliopiga marufuku mikutano ya kisiasa ya upinzani.