Monday, 29 August 2016

UDOM Kuziazima Wizara 4 Majengo Yake

Tarehe August 29, 2016
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani).V 1
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Hatimaye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimekubali kutoa majengo yake kutumiwa na wizara nne kama ofisi za muda wakati wakiendelea na ujenzi wa ofisi za kudumu Mkoani humo.

Hivi karibuni Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alikaririwa akisema kuwa suala hilo lisingewezekana kwani utaratibu huo ungeingiliana na taraibu za wanafunzi na kuvuruga hadhi ya elimu chuoni hapo.

Profesa Kikula amezitaja wizara hizo kuwa ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya majadiliano marefu na kukubaliana kuwa majengo mapya ambayo yalijengwa kwa ajili ya ofisi lakini kwa sasa hayatumiki ndio yatakayotumiwa na wizara hizo.

“Sasa wanaweza kutumia majengo hayo yaliyo mbali kidogo kwa muda wakati wakijenga ya kwao ya kudumu na hili halitaleta athari kwa wanafunzi kama ukosekanaji wa utulivu kwa wanafunzi kwakuwa yapo mbali kidogo,” amesema.

Ameongeza kuwa katika kufikia maamuzi hayo, wamezingatia pia umuhimu wa taasisi za Serikali kuunga mkono agizo la Rais Magufuli la kuhamia Mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuzingatia uwezekano wa majengo hayo kuharibika kutokana na kutotumiwa kwa muda mrefu kwa ajili ya shughuli za chuo.

Ameyataja majengo hayo kuwa ni pamoja na Kituo cha Utafiti cha Asha­Rose Migiro, na yale yaliyopo katika Chuo cha Sayansi ya Jamii (College of Humanities and Social Sciences).

Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza kuhamia Mkoani Dodoma ifikapo Septemba 1, mwaka huu ambapo alishaunda kikosi kazi kinachoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambacho kimebaini kuwa asilimia 70 tu ya majengo ya ofisi yataweza kupatikana huku asilimia 75 tu ya nyumba za kuishi watumishi ndizo zitakazopatikana.

clouds stream