Muhongo Ataka Matumizi Ya Teknolojia Ya Kisasa Katika Utafiti Wa Mafuta, Gesi
Tarehe February 23, 2016
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameyataka makampuni yanayojishughulisha na utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini kuongeza kasi ya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili sekta ya gesi na mafuta iweze kukua na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo ametoa kauli hiyo alipokutana na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya Schlumberger yenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na taasisi zake likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema Tanzania kwa sasa ina utajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi ambayo itachochea katika ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia umeme wa uhakika utakaotumika katika viwanda na kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania.
Aliendelea kusema kuwa ili sekta ya gesi na mafuta iweze kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwa kasi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Alisisitiza kuwa serikali ipo tayari kushirikiana na mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya gesi na mafuta kwa kutumia teknolojia ya kisasa.