Kazimoto Aomba Msaada Wa Wakili
Tarehe February 23, 2016
Kesi ya shambulio la kudhuru mwili inayomkabili kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto, imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga na kuomba msaada wa wakili.
Kazimoto ameshitakiwa kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Mwanahiba Richard na kesi yake ilianza kusikilizwa jana.
Akisomewa shitaka hilo, Mwanasheria wa Serikali, Upendo Shemkole, alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 10, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga, muda mfupi baada ya kumaliza mazoezi na timu yake ya Simba.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shitaka hilo na kuiomba mahakama kumpatia mwezi mmoja ili atafute wakili wa utetezi wake, ombi ambalo lilikubaliwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Rahim Mushi, anayesikiliza kesi hiyo, alisema kesi imeahirishwa hadi Machi 21 mwaka huu, itakaposikilizwa tena, ili kutoa fursa kwa mshitakiwa kupeleka wakili wake.
Jumla ya mashahidi sita wanatarajiwa kutoa ushahidi mahakamani hapo katika kesi hiyo, ambapo pia alipewa dhamana ya Sh 500,000.