Lowassa Agoma Kurudi CCM, Sasa Kuisuka Chadema
Tarehe February 6, 2016
Aliyekuwa Mgombea Urais kwa tiketi ya Ukawa Edward Lowassa amesema hana mpango wa kurejea katika chama chake cha zamani cha CCM badala yake ameanza mchakato wa kukisuka chama cha Chadema kujiandaa na uchaguzi mkuu wa 2020.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema licha ya kuitumikia CCM kwa zaidi ya miaka 30 tangu mwaka 1977, chama hicho kiliamua kutumia watu kumsakama kwa kila aina ya maneno jambo lililomfanya achoke na kuamua kuondoka.
“Nakifahamu Chama cha Mapinduzi, nakiheshimu kwani ndicho kilichonilea, lakini, kwa hali tuliyokuwa tumefikia, inafika mahali unasema imetosha,” alisema Lowassa.
Alitaja sababu nyingine iliyomfanya kuihama CCM kuwa ni kutaka mabadiliko na aliamini mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya chama hicho tawala na akisema hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema mabadiliko yatatafutwa hata nje ya CCM.
Akizungumzia kurudi CCM alisema kamwe hana mpango na hawezi kurudi CCM na akasema jukumu lililopo mbele yake kwa sasa ni kuijenga Chadema ambayo yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu.
Alisema yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, na jukumu lililoko mbele yake ni kukijenga na kukiimarisha chama cha Chadema hiki kiwe imara tangu katika ngazi ya matawi huku wakiwa wamejipanga kuzunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo pamoja na kuwashukuru nwananchi kwa imani waliyoionyesha kwake na chama chake.
Kwa upande wa Uchaguzi mkuu alisema kama si kura kuchakachuliwa, alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu wananchi walishaichoka CCM na wakawa wanataka mabadiliko.
Licha ya kukijenga Chama Lowassa alisema kazi nyingine kubwa waliyonayo sasa ni kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana na Tume ya Uchaguzi inaundwa upya kwani iliyopo si huru hata kidogo.