Serikali Yanuia Kufufua ATCL Ijiendeshe Kibiashara
Tarehe February 8, 2016
Serikali imesema ina mpango wa kulifufua upya Shirika la Ndege Nchini (ATCL) kwa kulinunulia ndege mpya na kulipa mtaji ili lifanye kazi kibiashara na kutengeneza faida kama ilivyokusudiwa awali.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokuwa anazungumza na Menejimenti na Wafanyakazi wa Shirika.
“Tutawekeza kwenye Air Tanzania ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuvutia wasafiri wengi kufika nchini moja kwa moja na kuvutia sekta ya utalii”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa pia amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo ambao sio waadilifu na wavivu kuondoka mara moja ili kupisha wafanyakazi wabunifu na wenye mawazo ya kibiashara kuendesha shirika hilo kwa faida.
“Tunataka watu watakaolitoa Shirika hili kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kuliwezesha kiuchumi na kujitegemea ili kushindana na mashirika mengine ya ndege katika biashara“,Prof. Mbarawa ameongeza.
Prof. Mbarawa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli yupo tayari kununua ndege mpya ili kulifufua Shirika na kuwataka wafanyakazi kuwa na mtazamo chanya wa kufanya biashara ili kuliletea Shirika tija na Taifa kwa ujumla.
Katika hali nyingine, Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaangalia upya taratibu za ajira katika shirika hilo na watakaobainika kuajiriwa kinyume cha taratibu watafukuzwa kazi mara moja.
“Tutanataka watu waadilifu, wabunifu na wenye sifa stahiki ili wafanye kazi kwa maslahi ya shirika na taifa kwa ujumla”, alifafanua Waziri Mbarawa.
Mapema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL , Bw. Johnson Mfinanga alisema kwa sasa Shirika hilo lipo katika hali mbaya kiuchumi na hivyo kuhitaji nguvu ya Serikali kulikwamua ili liweze kutoa huduma inayoshahili.
ATCL imekuwa ikijiendesha kwa hasara tangu mwaka 2009 na Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kulifufua shirika hilo ili lifanye kazi kwa faida na kuboresha usafiri wa anga ndani na nje ya nchi na hivyo kuvutia wasafiri wengi kuja nchini moja kwa moja.