Muuaji Kigogo Wa CUF Atoboa Siri Ya Aliyemtuma
Tarehe February 2, 2016
Kijana mmoja aliyefahamika kwaji na la Simon Shilage miaka 22 amekamatwa na jeshi la Polisi akidaiwa kushirikiana na mwenzake kumuua Diwani wa kata ya Kimwai huko Muleba Ndg. Faustine Muliga wa chama cha wananchi CUF.
Kwa mujibu wa Chanzo chetu kutoka Muleba kimebainisha kuwa kijana huyo alikamatwa jioni ya jana na wananchi wa kijiji cha Kyota akijaribu kutoroka akiwa na panga lenye damu alilotumia kumuua diwani Muliga.
Alipohojiwa kwa nini ametekeleza mauaji hao Simon amekiri kuwa kweli yeye na mwenzie mmoja (hakumtaja jina) ndio waliomuua Mhe. Muliga kwa kumkata mapanga akiwa nyumbani kwake wakati ana angalia taarifa ya Habari.
Kijana huyo amesema kazi hiyo ya mauaji hayo walitumwa na aliyekua mgombea udiwani wa Kata hiyo kwa tiketi ya CCM kwenye uchaguzi uliopita, ambaye alikua mpinzani wa Muliga lakini alishindwa kwenye uchaguzi.
Ameongeza kuwa Mgombea huyo aliwaahidi kiasi cha shilingi milioni 1.5 ikiwa watafanikiwa kumuua Muliga na aliwapa “advance” ya shilingi laki moja na nusu (150,000/=).
Baada ya makubaliano hayo vijana hao walimvamia Muliga nyumbani kwake majira ya saa 2 usiku akiangalia “Taarifa ya Habari” ambapo walimkata mapanga maeneo mbalimbali mwilini mwake kabla ya kutokomea kusikojulikana.
Imeelezwa kuwa Simoni alikamatwa na wananchi wenye hasira kali ambao walitaka kumuua ambapo wali mkata sikio na kisha akaokolewa na Polisi.
Mtuhumiwa huyo anashikiliwa kituo cha Polisi Muleba kwa upelelezi, kabla ya kupandishwa Mahakamani kujibu tuhuma za Mauaji.
Mtandao huu umemtafuta aliyekuwa mgombea udiwani anayedaiwa kuwatuma vijana hao bila mafanikio.