Mapya Yaibuka,Waziri Kuvujisha Ziara Ya Waziri Mkuu Kwa Meseji
Tarehe February 14, 2016
Mjadala mkali umezuka katika mitandao ya kijamii kuhusiana na nani hasa aliyevujisha ziara ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa Bandarini baada ya kubaini kuwepo zuio la kufunga kwa mita za mafuta kwa zaidi ya miaka mitano.
Katika ziara hiyo ambayo ni ya kushitukiza Waziri mkuu alibaini kuwa mita zilifungwa baada ya kuwepo taarifa kuwa yeye atafanya ziara ya kushitukiza katika eneo hilo.
Akiwa Bandarini hapo Majaliwa alikagua maeneo mbalimbali ndipo alipobaini kuwa mita za kupimia mafuta hazikuwa zinafanya kazi muda wa miaka 5 na zimeanza kufanya kazi siku moja kabla ya ziara yake.
Baada ya kumbana Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani, Bibi Magdalena Chuwa, ndipo amemtaja Waziri wa nishati na madini Prof Sospeter Muhongo kuwa ndiye aliyemtumia meseji akimpa maelekezo kwamba katika muda wa masaa 24 mita hizo ziwe zimefungwa na kuanza kufanya kazi.
Kufuatia sakata hilo la mita Serikali imewasimamisha kazi Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bernadina Mwijarubi.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika , Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
Waziri Mkuu pia alisema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.