Addo alipigania kurejeshwa kwa utawala wa vyama vingi
Kumeripotiwa ghasia nchini Ghana baada ya Tume ya uchaguzi kumtangaza Kiongozi wa chama cha NPP Akufo Addo kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Jumatano juma lililopita.
Mtu mmoja ameripotiwa kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa kutokana na ghasia hizo.
Wafuasi wa vyama vikuu viwili wanadaiwa kuhusika kwenye mashambulizi.
Kibanda kinachopokea malipo kwa ajili ya wapita njia kilichomwa moto mjini Brong Ahafo na jaribio la shambulio kama hilo lilifanywa katika mji wa Tema karibu na Accra.
Mwandishi wa Habari pia ameripotiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana mjini Accra.
Rais anayeondoka madarakani John Drama Mahama amelaani mashambulizi hayo na kuamuru Polisi kumkamata mtu yeyote aliyehusika na vitendo hivyo.
Chama cha NPP pia kimekemea mashambulizi hayo.
Polisi wametoa tahadhari kwa Umma kutojihusisha na vitendo vya vurugu.
Katika hatua nyingine, Rais John Dramani Mahama amezindua timu ya mpito inayoundwa na wanachama wa chama tawala na upinzani NPP.
Watafanyakazi pamoja kuhakikisha kuwa kuna makabidhiano ya madaraka kwa amani kutoka kwa Rais Mahama kwenda kwa Rais mteule, Akufo Addo wa NPP, ifikapo tarehe 7 mwezi Januari.