Mugabe anatarajiwa kupitishwa kugombea uchaguzi wa 2018
Migogoro ya ndani ya chama na kudorora kwa uchumi ni miongoni mwa ajenda kuu zinazotarajiwa kujadiliwa pindi Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atakapofungua mkutano wa mwaka wa chama chake hii leo.
Maelfu ya wafuasi waaminifu wa chama chake wamekuwa wakimiminika katika mji wa Masvingo umbali wa kilomita mia tatu kutoka kusini mashariki mwa mji mkuu.
Mkutano huo wa kila mwaka ni shughuli inayopendeza, huku ikihudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake, ambao huvaa nguo za chama rangi ya manjano na kijani.
Lakini je, mkutano huo utakaogharimu dola milioni tano utakuwa na manufaa gani?
Viongozi wa chama cha Zanu PF wamesema mkutano huo utaweka mikakati ya namna ya kufufua uchumi ambao umefifia.
Rais Mugabe nae anaonekana kuwa na matatizo yake, ikiwemo kukabiliana na wazee wa chama ambao wanaitolea macho nafasi yake.
Mikutano iliyopita, imekuwa ikigusia kuhusu sera za chama kuhusu uchumi, na kutaka kuondolewa kwa vikwazo vya uchumi huku wakithibitisha kumuunga mkono Rais Mugabe.
Chama kinatarajiwa kuja na makubaliano ya mwaka 2017 na kumthibisha Rais Mubage kupeperusha bendera ya chama kwa mwaka 2018.