Thomas
Mashali (kulia) akimuadabisha Dullah Mbabe jana usiku kweye pambano lao
la raundi 10, Mashali alishinda kwa pointi za majaji wawili kwa mmoja
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali ‘Simba asiyefugika’
jana usiku alimtwanga Abdallah Paazi ‘Dulla Mbabe’ kwa ushindi wa
pointi kwenye pambano la raundi 10 ambalo halikuwa la ubingwa
lililopigwa kwenye viwanja vya ndani vya Taifa.
Pambano hilo lililokuwa kali na lenye kuvutia, lilianza kwa kasi huku
Mashali akianza vyema pambano hilo kwa kumsukumia makonde mazito
mpinzani wake kwenye raundi za mapema. Mbabe nae hakuwa nyuma kwani
alikuwa akijibu mapigo na kulifanya pambano hilo kuwa la kuvutia zaidi.
Mashali ambaye ni mzoefu kwenye mchezo wa masumbwi, alionekana
kuchachamaa kuanzia raundi ya saba na kubadilisha kasi ya mchezo kitu
ambacho kilimchanganya Mbabe aliyeonekana kupungua kasi kadri muda
ulivyokuwa unayoyoma.
Wakali hao walitambiana kabla ya pambano lao hali iliyopelekea kutaka
kuzichapa ‘kavukavu’ siku ya Jumamosi walipokutana kwenye zoezi la
kupima uzito kabla ya pambano lao la jana.
Kwenye mapambano mengine ya utangulizi, Japhet Kaseba alikubali
kichapo kutoka kwa bondia Said Mbelwa, mpambano uliokuwa wa raundi nane
ambapo Mbelwa alishinda kwa pointi za majaji wa wili kwa mmoja.
Pambano jingine la raundi 10 liliwakutanisha Mada Maugo dhidi ya
Karama Nyilawila ambapo Maugo aliibuka mshindi kwenye pambano hilo kwa
pointi za majaji wawili kwa mmoja na kukata ngebe za nani mkali wa
kutupa makonde kati yao.
Pambno jingine la masumbwi la kimataifa litapigwa kati ya Mohamed
Matumla ‘Matumla Jr’ dhidi ya Wang Xin Hua kutoka China, pambano hilo
litachezwa Machi 27 kwenye ukumbi wa Diamond Jubelee jijini Dar es
Salaam.
Pambano hilo litakuwa la uzito wa Super Bantam kuwania nafasi ya
kwenda kugombea ubingwa wa taji la dunia la WBF kwenye mapambano ya
utangulizi Mei 2 mwaka huu huko Las Vegas Marekani siku ambayo kutakuwa
na pambano la Floyd Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao.