Sunday 6 March 2016

Chadema Waja Na ‘Dar Es Salaam Kuu’ Kuimaliza CCM ?

Chadema Waja Na ‘Dar Es Salaam Kuu’ Kuimaliza CCM ?

Tarehe March 6, 2016
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema Edward Lowassa.
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema Edward Lowassa.
Chama cha Chadema  kimesema kuwa kimeunda  chombo kipya cha uongozi katika jiji la Dar es salaam  na kukiita ‘Uongozi wa Dar es Salaam Kuu’.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu jana jijini hapa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chombo hicho kipya kitaongozwa na Mweyekiti Bw. Mwita Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga.
Amesema wameunda chombo hicho kwa mujibu wa Ibara ya 6.1.3 ya katiba ya chama hicho ili kurejesha demokrasia iliyopotea katika Jiji la Dar es salaam.
Ibara hiyo inasema; Kwa kuzingatia ibara ya 6.1.2, ngazi ya juu ya chama itateua kamati ya muda itakayokuwa na wajibu wa kuratibu shughuli za chama na kuwaunganisha wanachama katika eneo lisilo na uongozi wa kikatiba mpaka watakapofikia uwezo wa kuwa na uongozi wa kikatiba.
Mbowe amesema mikoa hiyo ya kichama ya Kinondoni, Ilala na Temeke, itakuwa na chombo kitakachoiunganisha ambacho ni uongozi wa Dar es Salaam Kuu ambao kazi yake ni   kuongeza nguvu, usimamizi na uratibu wa operesheni za chama.
Amesema chombo hicho kitakuwa na wajumbe wasiozidi 25 na uongozi wa chama hicho katika mikoa ya Kinondoni, Temeke na Ilala utabaki vilevile.
Ameongeza kuwa  kamati inayounda chombo hicho itawahusisha wabunge wote wa kuchaguliwa na wa viti maalumu wa Chadema mkoani humo na mameya wa Ilala na Kinondoni.
Wabunge hao ni Mdee, John Mnyika (Kibamba), Waitara, Saed Kubenea (Ubungo), Susan Lyimo, Anatropia Theonist na Lucy Mollel
Uundwaji chombo unafuatia Chama hicho  kuwa na uhakika wa kushinda uchaguzi wa meya wa jiji hilo kwa ushirikiano na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ikilinganishwa na CCM.
Akizungumzia utata katika uchaguzi wa Meya jijini hapa Mbowe amesema uchaguzi huo umeahirishwa mara tatu na ya mwisho kwa kutumia zuio ‘batili’ la Mahakama  kumezua mtafaruku kati ya wabunge na wadiwani wa chama hicho dhidi ya polisi.
Hadi sasa  wabunge wawili, Halima Mdee na Waitara pamoja na madiwani watatu wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kumshambulia Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando ambaye alikuwa msimamizi wa uchaguzi huo.
Wagombe  katika nafasi ya umeya wa Jiji ni pamoja na Yesaya Mwita, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob.

clouds stream