Mkurugenzi Mstaafu, Mameneja 9 ‘Watumbuliwa’ Dawasco
Tarehe March 12, 2016
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ametangaza kuwasimamisha kazi mameneja tisa wa Shirika la Majisafi na Majitaka la Dar es Salaam (Dawasco), pamoja na mkurugenzi aliyestaafu kwa tuhuma za kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh 2.8 bilioni.
Kwa mujibu wa Waziri Lwenge alisema kusimamishwa kwa watumishi hao ni kutokana na kutuhumiwa kushiriki katika njama za kuiunganisha maji kampuni ya Strabag bila kufuata utaratibu.
Watumishi waliosimamishwa ni Peter Chacha, Regnald Kessy, Theresia Mlengu, Josper Kilango, Fred Mapunda, Mvano Mandawa, Emanuel Gulupa, Raymond Kapyela na Jumanne Mapunda.
Licha vigogo hao Waziri Lwenge pia ameagiza aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo ambaye alistaafu, Jakson Midala naye achunguzwe ushiriki wake katika njama hizo kwa kuwa zilifanyika wakati wa uongozi wake.
Aidha, waziri huyo wa maji ametoa siku 14 kwa Strabag kulipa kiasi hicho cha pesa kilichokwepwa vinginevyo hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo.
Akizungumzia jinsi maji yalivyoibwa Waziri alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu wa shirika hilo la maji walifanikisha kuunganisha maji bila kupata vibali na kufuata utaratibu.
Alisema baada ya kuunganishiwa maji, Strabag walianza kuyatumia katika ujenzi wa barabara hizo bila kuyalipia na kulikosesha shirika mapato yake. Unganisho hilo lilifanyika mwaka 2014 kutoka kwenye mabomba yenye vipenyo vikubwa (DN 100 na DN 400).
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema changamoto kubwa inayolikabili shirika hilo ni upotevu wa maji ambao mbali na wezi, pia unasababishwa na uchakavu wa mitambo ambayo mingi ni ya miaka 1970.