Maalim Seif Atua Z’bar, Adai Polisi Sasa Ni Tawi La CCM
Tarehe March 5, 2016
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyewasili jana Zanzibar kutoka nchini India kwa matibabu amelishushia lawama Jeshi la Polisi visiwani humo kuwa limegeuka tawi la CCM.
Akizungumza na wafuasi wake waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na baadaye kumsindikiza hadi nyumbani kwake Mbweni mjini hapa Maalim amedai kusikitishwa na kuona hujuma, watu wakipigwa na kujeruhiwa na Mazombi kila kukicha wakati Polisi wapo wanayaona na hakuna aliyeitwa kuhojiwa.
Aiidha, Maalim Seif alimlaumu, Dk Ali Mohamed Shein kuwa si muungwana akidai kuwa amekataa kuondoka madarakani.
Alisema la kushangaza zaidi ni kuona aking’ang’ania uchaguzi wa marudio, ilihali hakuna mantiki wala kifungu chochote cha sheria kinachohalalisha hatua hiyo.
Baadhi ya viongozi wa CUF waliohudhuria mapokezi hayo ni pamoja na Mansour Yussuf Himid, Nassor Ahmed Mazrui, Fatma Abdulhabibi Ferej na aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema chini ya mwavuliwa wa Ukawa katika urais wa Muungano, Juma Duni Haji.
Maalim Seif pia alimtahadharisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha asijaribu kulazimisha chama hicho kushiriki uchaguzi ‘batili’ wa marudio.
Uchaguzi wa marudio visiwani humo umepangwa kufanyika machi 20 mwezi huu,huku serikali ya Zanzibar ikisema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri.