Zitto Kabwe Ajiuzulu Kamati Ya Bunge Kisa Tuhuma Za Rushwa
Tarehe March 22, 2016
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ametoa taarifa rasmi ya kujiuzulu kutoka kwenye kamati aliyokuwa akihudumu ya Huduma za Maendeleo ya Jamii kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha uliotokana na rushwa.
Kupitia mtandao wa kijamii Zitto Kabwe, ameandika ujumbe kutoa taarifa hiyo, na kusema kuwa pia ameamua kufanya hivyo ili kupisha uchunguzi kufanyika.
Sambamba na hilo amedai kuwa amemuandikia barua spika wa bunge ili uchunguzi huo ufanyike kwa haraka dhidi ya tuhuma hizo na ikiwezekana hatua kali dhidi ya yeyote atakayehusika na vitendo vy rushwa ichukuliwe.
“Kuna tuhuma za rushwa dhidi ya kamati mbalimbali za Bunge, ikiwemo kamati ninayohudumu. Nimemwandikia Spika kuomba uchunguzi juu ya tuhuma hizo na kwamba achukue hatua kali dhidi ya yeyote atakayekutwa kuhusika na vitendo vya rushwa, nimejiuzulu ujumbe wa kamati ili kutoa nafasi ya uchunguzi husika”, aliandika Zitto
Mapema mwaka huu wabunge waliteuliwa kuhudumu kwenye kamati mbali mbali, na Zitto Kabwe, alipangwa kwenye kamati ya Huduma na maendeleo ya jamii, ambapo awali alikuwa akihudumu kwenye kamati ya hesabu za serikali (PAC).