Mwapachu Atoa Siri Ya Lowassa, Arejea Rasmi CCM
Tarehe March 16, 2016
Kada mkongwe Balozi Juma Mwapachu aliyetangaza kukihama chama cha Mapinduzi kwa mbwembwe tarehe 13 Oktoba 2015 leo amerejea nyumbani katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuatia chama chake kuteua mgombea ambaye ni Rais Magufuli aliyeibadilisha nchi kwa kipindi cha muda wa miezi 3 na siku kadhaa.
Kada huyo aliyetangaza kuihama CCM na kurejesha kadi yake ya uanachama katika ofisi ya CCM Kata ya Mikocheni leo amerudi katika tawi hilo la CCM na kuichukua kadi yake.
Akizungumza baada ya kuchukua kadi yake amesema kwamba hapo mwanzo aliamini kuwa CCM imepoteza mwelekeo kwa kuamua kumnyima haki ya kugombea mcha mungu Edward Lowassa ambaye yeye alikuwa rafiki yake wa karibu.
“Baada ya miezi miwili ya uongozi wa Magufuli nataka niseme nilikosea sana. Nililewa mahaba ya Lowasa na nilipotezwa na ahadi ya Lowasa ya kunipa uwaziri wa mambo ya Nje.” Amesema Mwapachu.
Ameongeza kuwa aliamini mafuriko ya Lowasa ambayo yalimfanya aamini kabisa anachukua nchi na kunyetisha kuwa walikubaliana na wenzake kwamba wiki mbili za mwisho tuihame CCM kwa wimbi kubwa ili kuitikisa na kukitoa madarakani chama kikongwe cha Mapinduzi CCM, ambapo baadhi waliogopa na hadi sasa bado wamebaki CCM na wana vyeo.
Mwapachu amesema ameamua kurudi CCM kwasababu ameona kazi nzuri ya Magufuli na kujutia kosa kubwa alilolifanya katika siasa la kuihama CCM na kuwasihi vijana walio kwenye siasa wasilifanye.
“Nilihama kwa kwasababu ya mtu (Lowassa). Nimerudi kwasababu ya mtu (Magufuli). Nataka niwaahidi kwamba CCM ikiweka mtu hovyo baada ya Magufuli, sitahama,”Ameongea Mwapachu
Ameomba radhi familia ya baba wa taifa Mwalimu Nyerere kwa kuitumia kisiasa siku aliyokufa (tar 14 Octoba) na kutumia msiba wake kutoa kauli za kisiasa dhid ya chama chake alichokiunda na ambacho hadi anakufa alikuwa mwanachama.