Monday 7 November 2016

Benki Ya Twiga Kuanza Huduma Kesho Baada Ya Tathmini Kukamilika

twiga
V 2

Kwa mamlaka iliyopewa kisheria kupitia kifungu namba 58(2) (a) na (b) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu inapenda kuutarifu umma kwamba zoezi la tathmini ya hali ya kifedha ya Twiga Bancorp Ltd (Twiga) limekamilika; kwa mantiki hiyo, Twiga itaanza kutoa baadhi ya huduma za kibenki kwa umma kuanzia Jumanne tarehe 8 Novemba 2016.

Huduma hizo ni pamoja na ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya wateja. Meneja Msimamizi wa benki hiyo atawajulisha wateja huduma zitakazotolewa na taratibu za kuzingatia.

Benki Kuu ipo katika mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili Twiga Bancorp. Njia inayopewa kipaumbele ni kutafuta mtaji kutoka kwa wawekezaji wapya, mchakato utakaowahitaji kuchambua hali halisi yataarifa za hesabu za Twiga (due diligence).

Zoezi hili linatarajiwa kuchukua takribani wiki tatu na litakapokamilika, Benki Kuu itaingia makubaliano na wawekezaji wapya kuhakikisha wanaingiza mtaji unaohitajika haraka iwezekanavyo ili shughuli za kawaida za kibenki ziweze kuendelea. Benki ya Twiga itaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu hadi hapo utaratibu wa kuwamilikisha wawekezaji wapya utakapokamilika.

Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza kuiweka Twiga Bancorp Ltd chini ya usimamizi wake kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016 kutoka na upungufu mkubwa wa mtaji unaoikabili.

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

BENKI KUU YA TANZANIA 6

Novemba, 2016

clouds stream