Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA, Edward Lowassa.
Aliyekuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewashukuru wananchi kwa kumpigia kura kwa wingi licha ya baadhi kumsema vibaya kwa kumwita mgonjwa na kwamba angekufa.
Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, ametoa kauli hiyo Mjini Mbinga Mkoani Ruvuma ambako chama hicho kipo katika ziara ya kufanya mikutano ya ndani.
Pasipo kutaja jina la mtu, Lowassa amesema Mwacheni Mungu aitwe Mungu, kwa sababu wote hata walionisema mabaya baadhi yao wameshatangulia mbele ya haki.”
Amesema kitendo cha wananchi kumpigia kura kwa wingi pamoja na kwamba alikuwa akizungumziwa vibaya juu ya afya yake, ni wazi kuwa walikubali kubeba lawama juu yake.
“Bila ujasiri na umoja wa dhati, hawa jamaa wataendelea kutupiku… lakini niwashukuru vile vile kwa kukubali kubeba lawama juu yangu, wapo waliosema huyu ni mgonjwa atakufa, bado mlinipigia kura nyingi ila Mungu ndiye hupanga yote,” amesema.
Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa Zamani amewataka wanachama wa Chadema kuendelea kuwa na ujasiri na kudumisha umoja kwa kuendelea kujipanga kwa uchaguzi wa mwaka 2020.
Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumza juu ya watu ambao walihoji kuhusu mwenendo wa afya yake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.