Mtu mweusi nchini Afrika Kusini ambaye alidaiwa kulazimishwa kuingia katika jeneza na wakulima wawili weupe kwa kupita katika shamba lao amesema kuwa anahofia maisha yake.
Victor Mlotshwa alikuwa akizungumza nje ya mahakama ya mji wa kaskazini mashariki wa Middelburg ambapo waliotaka kumshambulia waliwasilishwa katika mahakama.
''Nilidhani wataniua'',alisema.
Kanda ya video ya dakika 20 iliorekodi kisa hicho imekuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii nchini Afrika Kusini.
Mwandishi wa BBC Pumza Fihlani huko Middelburg anasema kuwa ndani ya mahakama hiyo ,washtakiwa hao ,Theo Martins Kackson na Willem Oosthuizen,walisimama wakiwa wameinamisha vichwa vyao chini huku waandishi wa habari na raia wakichukua picha zao.
Wameshtakiwa kwa kumteka nyara na kumshambulia kwa lengo kumjeruhi vibaya.Hawajakubali ama kukana mashtaka hayo.
Wawili hao wanazuiliwa hadi tarehe 25 Januari huku waendesha mashtaka wakisema kwamba walihitaji muda zaidi kuchunguza ,ikiwemo kuthibitisha video hiyo.
Mamake bw Mlotshwa alijawa na hasira na kushindwa kujizuia wakati wa kusikizwa kwa kwesi hiyo.Nje ya mahakama kulikuwa na kelele za wafuasi wa vyama vikuu nchini humo huku #RacismMustFall ikisambazwa katika mitandao ya kijamii.